Kocha msaidizi wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Selemani Matola, amesema wamepoteza mechi kwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia kwa makosa ya kimpira tu na wala si kuzidiwa kama inavyoelezwa na baadhi ya mashabiki
Akizungumza nchini Cameroon baada ya mechi iliyochezwa mjini Limbe juzi, Matola alisema walifungwa bao la penalti ambayo ilitokana na makosa ya kimchezo, ambayo ndiyo yalisababisha hata kupatikana kwa bao la pili.
"Tumepoteza mechi, wachezaji wetu walicheza vizuri sana vipindi vyote viwili, siyo kipindi kimoja tu kama inavyosemwa. Tatizo ni kwamba lilikuwa ni kosa tu la bahati mbaya mpira ulimgonga Shomari Kapombe mkononi ikapatikana penalti, wakaitumia, hivyo ndiyo iliyosababisha wachezaji wetu wahamaki na kutaka kurudisha bao, lakini waliacha mianya ambayo Zambia waliitumia kutuadhibu bao la pili," alisema Matola ambaye ni mchezaji wa zamani wa Taifa Stars
Matola ameahidi kuwa watarekebisha makosa hayo ili kushinda kwenye mechi inayofuata dhidi ya Namibia