Beki Shomari Kapombe ambaye alikuwa nahodha wa kikosi cha Stars kilichoshuka dimbani jana kucheza na Zambia, amesema walipoteza mchezo huo kutokana na kupoteza umakini katika kipindi cha pili
Stars ikiwa na kikosi chenye sura ngeni nyingi, walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa hawajafungana na Zambia lakini kwenye kipindi cha pili wakaruhusu mabao mawili
"Naweza kusema ni matokeo ya mchezo tu, dhamira yetu ilikuwa kupata ushindi lakini tulifanya makosa na wapinzani wetu wakatumia makosa hayo kutuadhibu"
"Tulitawala mchezo katika kipindi cha kwanza lakini tukapoteza umakini kwenye kipindi cha pili hivyo kupelekea tukapoteza mchezo. Naamini kocha ameona mapungufu yaliyojitokeza na ataweza kuyasahihisha ili tuweze kufanya vizuri michezo iliyobaki," alisema Kapombe
Tanzania ilifungwa mabao 2-0 na Zambia katika mchezo wa kwanza wa kundi D uliopigwa jana usiku
Matokeo hayo yatailazimu Tanzania angalau kushinda mechi zote mbili zilizobaki dhidi ya Guinea na Namibia ili kutinga raundi ya pili
Hata halitakuwa jambo rahisi kwani Guinea kikosi chao kinaonekana kuwa imara pengine kuliko hata Zambia
Guinea inaongoza kundi baada ya kuichapa Namibia mabao 3-0 wakifuatiwa na Zambia