Bado matukio ya vurugu viwanjani yanaendelea kushamiri baada ya juzi Mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzalez kufanyiwa vurugu na watu wasiojulikana usiku baada ya Simba kumaliza mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo dhidi ya Yanga uliopigwa jana uwanja wa Amaan
Barbara alikumbwa na mkasa huo uwanja wa Amaan wakati akiswali swala ya Isha saa mbili usiku
Tukio hilo liliripotiwa kituo cha Polisi N'gambo na washukiwa kadhaa wamekamatwa
"Wakati naswali walikuja watu wakaanza, kunivuta mtandio wangu na kunipiga. Nilipata maumivu makali. Niliripoti tukio hilo kituo cha Polisi N'gambo na kufunguliwa jalada lenye namba NGB/RB247/2021," alisema Barbara
Awapongeza wachezaji Simba
Katika hatua nyingine, Barbara amewapongeza wachezaji wa Simba kwa kufanikiwa kucheza fainali ya michuano ya kombe la Mapinduzi licha ya kufungwa na watani zao Yanga kwa mikwaju ya penati 4-3
Barbara amesema uongozi wa Simba umeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu katika michuano hiyo ambayo Simba imetoa mfungaji bora, Miraji Athumani aliyefunga mabao manne na mchezaji bora wa mashindano, Francis Kahata
"Nawapongeza wachezaji wamefanya kazi kubwa. Tumecheza mechi nne katika kipindi cha siku sita, lakini vijana wamepambana sana"
"Pamoja na kuwa hatukushinda mchezo wa mwisho, sisi tumeridhishwa na juhudi zilizoonyeshwa na wachezaji wetu hatuwezi kuwalaumu kwa kupoteza mchezo wa fainali," alisema Barbara