Saa 11 jioni, leo Jumatano Januari 06, mabingwa wa soka Tanzania Simba wana jambo lao pale uwanja wa Benjamin Mkapa wakisaka ushindi muhimu dhidi ya Fc Platinum utakaowapeleka hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Baada ya Namungo Fc kufanikiwa kutinga raundi ya pili ya michuano ya kombe la Shirikisho kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-3 dhidi ya El Hilal Obeid ya Sudan, Machampioni wa soka nchini Simba leo ni zamu yao, wana kila sababu ya kupata ushindi dhidi ya Fc Platinum
Wanacheza kwenye ardhi ya nyumbani, muhimu zaidi wanacheza mbele ya mashabiki wao zaidi ya 30,000 ambao wataruhusiwa kuingia uwanjani kuushuhudia mchezo huo
Ushindi wa kuanzia mabao 2-0 utatosha kuivusha Simba hatua ya makundi na kuipaisha Tanzania Kimataifa
Ni War in Dar (WIDAR), hii ni mechi ya lazima kwa Simba kushinda baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kule Zimbabwe
Kikosi cha Simba kimejiandaa kikamilifu, wachezaji wana kazi moja tu ya kuhakikisha wanafanikisha lengo la kwenda makundi
Mara nyingi, wababe hao wa soka nchini wanapocheza uwanja wa Benjamin Mkapa tena mbele ya mashabiki wao, wanakuwa 'wanyama' kwelikweli
Ndio maana kila Mwanasimba leo anasubiri kushangilia ushindi baada ya dakika 90 au 120, vyovyote itakavyokuwa lazima mnyama atakate
Dua ya kila Mtanzania mzalendo, shabiki wa Simba inahitajika sana kuhakikisha lengo la kucheza makundi linafanikiwa
Ni saa 11 jioni ya leo pale uwanja wa Benjamin Mkapa, ni War in Dar (WIDAR)...