Afisa Habari wa klabu ya Simba Haji Manara amesema uongozi umeandika barua kwa shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) wakiomba kuongezewa idadi ya mashabiki kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Fc Platinum ambao utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa wiki ijayo
CAF iliruhusu Tanzania kuingiza mashabiki nusu uwanja katika michuno yake baada ya kujiridhisha kuwa kwa Tanzania hakuna changamoto kubwa ya ugonjwa wa corona
Tanzania ndio nchi pekee barani Afrika ambayo CAF imetoa ruhusa iingize mashabiki viwanjani
"Tumewaandikia barua CAF tukiwaomba waturuhusu tuingize mashabiki kwa asilimia 100% katika mchezo wetu. Hapa Tanzania sisi hatuna corona hivyo tunaamini ombi letu litakubaliwa, tunasubiri watujibu"
"Mashabiki wamekuwa chachu kubwa kwetu kufanya vizuri katika michuano mbalimbali. Mara nyingi huwa nasema mastaa katika klabu yetu sio akina Chama, ni hawa mashabiki. Na ndio maana wakati huu tumewapa ofa ya kununua tiketi kwa bei punguzo," Manara aliiiambia Azam TV
Aidha, Manara ambaye ametokea kwenye fungate baada ya kufunga ndoa hivi karibuni, amewataka Watanzania wote wakiwemo watani zake Yanga kuiombea Simba iweze kutinga makundi kwani kwa kufanya hivyo manufaa yatakuwa kwa wote
"Sisi mkakati wetu haujabadilika, tutashinda ubingwa wa ligi kuu kwa miaka 10 mfululizo, hivyo kila mwaka tutacheza ligi ya mabingwa. Sasa njia pekee kwa wengine kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo ni kutuombea na kutushangilia ili tufanye vizuri tuongeze idadi ya timu zinazokwenda kushiriki kama ilivyokuwa msimu uliopita"
"Kwa hiyo uamuzi ni wao, watuombee ili tuwabebe au wasituombee ili mwakani wao wasishiriki kwani nina uhakika tutarudi sisi kwa mara nyingine. Tutafanya hivyo kwa miaka 10 mfululizo...!," alitamba Manara