Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama ndiye mchezaji anayeonekana kubeba majukumu ya ushindi wa Simba kwa sasa.
Simba, ambayo inatakiwa kushinda dhidi ya FC Platnum ya Zimbabwe Januari 6, itamhitaji zaidi kiungo huyo wa kimataifa wa Zambia kuwa fiti kwa asilimia 100.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walipoteza kwa bao 1-0 kule Zimbabwe katika mchezo wao wa kwanza waLigi ya Mabingwa Afrika wakisaka nafasi ya kutinga makundi.
Ni wazi kwa sasa Chama amekuwa mchezaji muhimu sana ndani ya kikosi cha Simba na anatimiza ipasavyo wajibu wake
Katika mechi tatu za Ligi Kuu zilizopita, Chama alionyesha umuhimu wake akiingia kipindi cha pili mechi dhidi ya Polisi Tanzania na kufunga mabao yote mawili kwenye ushindi wa Wekundu wa Msimbazi wa mabao 2-0.
Kiungo huyo pia alitoa pasi ya bao kwenye mchezo uliofuata dhidi ya Mbeya City lililofungwa na John Bocco, wakati Simba ikishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mchezo uliofuata wa Ligi Kuu ulikuwa dhidi ya KMC, ambao Simba ilishinda bao 1-0 kwa mkwaju wa penalti ya Meddie Kagere
Kimataifa hadi sasa Simba imecheza mechi tatu, mbili dhidi ya Plateau United ya Nigeria na ile dhidi ya Platnum ya Zimbabwe. Simba imefunga bao moja katika mechi hizo tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika, ambalo pia limefungwa na Chama nchini Nigeria.