Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba Ismail Aden Rage amesema mabingwa hao wa nchi hawapaswi kuidharau FC Platinum ambayo watachezanayo kesho mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kufuzu kucheza hatua ya makundi
Rage amesema timu hiyo inaonekana kuwa imara zaidi kulinganisha na wapinzani wa Simba waliopita Plateau United ya Nigeria
"FC Platinum si timu ya kuibeza, ni timu nzuri na kuna mchezaji alikuwa Ulaya (Silas Songani) amerudi pale. Zimbabwe ina mchezaji ambaye anacheza Aston Vila (Marvelous Nakamba) kwa hiyo kama nchi pia wapo vizuri."
"FC Platinum inaongoza ligi ya Zimbabwe ikiwa na pointi 62 timu ambazo maarufu Zimbabwe ni Highlanders ya Bulawayo ipo nafasi ya 6 na Dynamos ipo nafasi ya 9 kwa hiyo utaona ubora wao."
"Wana rekodi pia kwenye mashindano ya Afrika, wameingia mara sita, mara nne wametolewa hatua za mwanzo, mara mbili wametolewa kwenye hatua ya makundi. Hatutakiwi kuwabeza hata kidogo ni timu nzuri kuliko ile timu ya Nigeria (Plateau United) huo ndio ukweli," alisema Rage
Mchezo baina ya timu hizo utapigwa kesho kuanzia saa kumi kamili jioni katika uwanja wa Taifa wa Zimbabwe