Wakati wakitarajia kushuka dimba la Taifa la Zimbabwe keshokutwa, Jumatano kuwavaa wenyeji wao, FC Platinum kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, beki 'mmwaga maji' wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe, amesema watapambana kutafuta matokeo mazuri katika mchezo huo, ili kurahisisha kazi watakaporudia.
Beki huyo mahiri amesema anaamini mchezo huo utakuwa na ushindani mkali kwa sababu kikosi cha FC Platinum kinaundwa na baadhi ya nyota waliowahi kucheza soka Tanzania.
Kapombe amesema uwapo wa nyota kama Thabani Kamusoko aliyewahi kuichezea Yanga, Donald Ngoma (Yanga na Azam) pamoja na Elias Maguri ambaye naye aliwahi kuichezea Ruvu Shooting, Simba, Stand United na KMC FC, kutauongeza ushindani katika mchezo huo.
"Itakuwa mechi ya ushindani ukizingatia nyota hao tumewahi kucheza nao katika ligi na timu moja, hivyo tunajuana vizuri, lakini tutapambana kutafuta matokeo chanya kuhakikisha tunafikia kile kinachotarajiwa na Wanasimba," alisema Kapombe.
Beki huyo aliwataka mashabiki kuendelea kuwasapoti katika kila mechi na wao watahakikisha wanapambana kutafuta matokeo mazuri na ikiwezekana kumaliza kazi ugenini kabla ya kurejea nyumbani katika mchezo wa marudiano.
Simba ambayo imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa Plateau United ya Nigeria kwa bao 1-0, tayari ipo Harare, Zimbabwe tangu wiki iliyopita ikijiwinda kwa mechi hiyo kabla ya kurudiana Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kati ya Januari 5-6, mwakani.
Endapo itaitoa FC Platinum, itatinga moja kwa moja hatua ya makundi na mechi za kwanza zitaanza kupigwa Februari mwakani.
Mchezo huo utachezwa Jumatano, Desemba 23 ambapo utakuwa ni wa raundi ya kwanza na ule wa marudio unatarajiwa kuchezwa Dar, Januari 6.
FC Platinum imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa Costa do Sol ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 4-1 ikishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani