Mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzalez amesema wamepata mapokezi ya kiungwana nchini Zimbabwe ukilinganisha na walipokwenda Nigeria kucheza na Plateau United
Barbara ambaye alitangulia nchini Zimbabwe amesema kwa kushirikiana na Balozi wa Tanzania nchini humo wameonyeshwa sehemu nzuri na tulivu kwa ajili ya timu hiyo itakapofikia na kufanyia mazoezi kabla ya siku ya mechi.
"Huku hakuna vurugu kama tulizofanyiwa Nigeria, kumepoa hadi sasa hatujaona zile fujo au figisufigisu kutoka kwa wenyeji wetu, tuna imani utakuwa mchezo mzuri na ushindani mkubwa," alisema Barbara
Simba iliwasili nchini Zimbabwe jana mchana, wakapokewa na ubalozi wa Tanzania nchini humo
Wachezaji waliosafiri kwa ajili ya mechi hiyo ni makipa Aishi Manula, Ally Salm na Beno Kakolanya; Mabeki ni Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Erasto Nyoni, Ibrahim Ame, Joash Onyango na Pascal Wawa.
Kwa upande wa viungo ni Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Said Ndemla, Taddeo Lwanga, Rally Bwalya, Hassan Dilunga, Francis Kahata na Clatous Chama, huku washambuliaji wakiwa ni John Bocco, Meddie Kagere, Chris Mugalu, Miraji Athumani, Luis Miquissone na Ibrahim Ajibu.