Mlinda lango wa Simba Aishi Manula amesema wamekwenda nchini Zimbabwe wakiwa na lengo moja, tu kuhakikisha wanaipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi ya mabingwa dhidi ya Platinum Fc
Manula akiwa miongoni mwa wachezaji 24 walioondoka nchini mapema siku ya Ijumaa na kuwasili salama kule Zimbabwe, amesema kila mchezaji anafahamu malengo yaliyowekwa mbele yao hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanapata matokeo ambayo yatawapa furaha mashabiki wao
Kipa huyo namba moja hapa nchini, amesema michuano ya ligi ya mabingwa ina ushindani mkali lakini kinachowapa matumaini ya kufanya vizuri ni ubora wa kikosi chao ambacho kimesheheni wachezaji wenye uwezo na wanaojitoa kwa ajili ya timu
"Kama wachezaji, tumekubaliana kufanya makubwa katika michuano ya mwaka huu. Tutapambana ndani ya uwanja kuhakikisha tunalifanikisha hilo.
"Tumejiandaa vizuri, kila mmoja yuko tayari na tunafahamu huku nyumbani mashabiki wetu watakuwa nasi bega kwa bega kwa dua na sala ili tufanye vizuri," alisema Manula muda mfupi kaba ya kuondoka nchini
Mchezo dhidi ya Platinum Fc utapigwa Jumatano, Disemba 23 huko Zimbabwe na mchezo wa marudiano kupigwa wiki mbili baadae uwanja wa Benjamin Mkapa
Simba imewasili mapema Zimbabwe ili kupata nafasi ya kuzoea hali ya hewa, wakiwa na takribani siku nne za kujifua kabla ya mchezo huo