Baada ya kufanya mazoezi kwa muda mfupi na kuonyesha uwezo mkubwa, kiungo mpya wa Simba raia wa Uganda, Taddeo Lwanga ametajwa kuwa mrithi halisi wa Gerson Fraga
Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck ameeleza kuvutiwa na kiungo huyo baada ya kumshuhudia mazoezini
Sven amemwagia sifa Lwanga kuwa ametimia kila idara hasa katika eneo la ukabaji jambo ambalo litaipa Simba uwiano nzuri kama ambavyo alikuwa akifanya Fraga na akiongeza kuwa Jonas Mkude atakuwa na muda wa kutimiza majukumu yake kwa asilimia 100 kwa kuwa amepata mtu sahihi wa kumsaidia
Fraga aliumia goti ambalo alifanyiwa upasuaji na anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda wa zaidi ya miezi sita hivyo Simba ikalazimika kumsajili Lwanga
"Nimemtazama Lwanga kwa wakati mfupi aliofanya mazoezi na timu, akili yake ya kukaba na kukaa na mpira ni kubwa sana, mwili wake una nguvu sana, naamini lile pengo la Fraga litakwenda kuzibwa, lakini kitu kizuri zaidi Mkude amepata mtu wa kusaidiana naye kwani alikuwa peke yake kwa kipindi kirefu kidogo," alisema Sven
Lwanga ataanza rasmi kuitumikia Simba baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Jumatano ijayo