Shoo ya takribani dakika 30 kutoka kwa Clatous Chama 'Mwamba wa Lusaka' ilitosha kuihakikishia Simba ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Kocha Sven Vandenbroeck alifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake kwenye mchezo wa leo akiwapumzisha wachezaji muhimu ambao walitumika zaidi katika michezo iliyopita
Hata hivyo mpango huo uliiathiri Simba kwa kiasi fulani, kwani mabingwa walilazimika kusubiri mpaka dakika ya 65 kuandika bao la kuongoza kupitia kwa Chama ambaye aliweka mpira kambani baada ya dakika mbili tu toka alipoingia!
Fundi huyu aliichangamsha zaidi Simba, dakika za majeruhi akaongeza bao la pili lililoihakikishia Simba alama tatu muhimu zilizowafanya wafikishe alama 26
Chama sasa amefikisha mabao 6 na kuwa kiungo pekee anayechuana na washambuliaji katika kuwania kiatu cha dhahabu
John Bocco anaongoza mbio hizo akiwa ameweka kambani mabao saba
Kwa hakika Chama ni Simba na Simba ni Chama, Mwamba wa Lusaka ameendelea kuwapa furaha Wanamsimbazi
