Kiungo mpya wa Simba sc Mganda Taddeo Lwanga amesema kuwa klabu hiyo ina viungo wengi wazuri lakini anaamini kuwa atapambana na kufanikiwa kupata nafasi katika kikosi Cha klabu hiyo
Lwanga aliyesajiliwa na Simba wiki iliyopita kuchukua nafasi ya majeruhi Gerson Fraga, amesema anafahamu atahitaji kupambana ili kuweza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza
"Nimeona Simba kuna viungo wengi wazuri na mpaka unapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza au kuingia kuna kazi kubwa ambayo mchezaji unatakiwa kuifanya katika mazoezi ili kupewa mechi," alisema mchezaji huyo wa zamani wa Tanta ya Misri.
"Ukiangalia katika mechi na Plateau nafasi ya kiungo mkabaji walicheza Jonas Mkude na Mzamiru Yassin ambao walitimiza majukumu vizuri ya kazi yao, lakini ukiachana na hao kuna viungo wengine kama Said Ndemla na Larry Bwalya hawakutumika lakini wapo katika viwango bora.
"Ubora wa viungo na wachezaji wote wa Simba nalifahamu hilo na nipo tayari kwa kushindana na kuna kitu ambacho nitajitahidi kuongeza katikati kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, kwani wote tuna malengo ya kuhakikisha tunapambana kwa ajili ya timu na kuifikisha mbali," aliongeza Lwanga