Mfungaji bora wa Simba misimu miwili mfululizo Meddie Kagere amewaibua mashabiki baada ya mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Plateau United uliopigwa jana uwanja wa Benjamin Mkapa na kumalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila ya kufungana
Msimu huu Kagere amekuwa na wakati mgumu kupata nafasi kwenye kikosi cha kocha Sven Vandenbroeck ambaye mfumo anaotumia hutegemea mshambuliaji mmoja
Pamoja na kulazimishwa suluhu jana, mabingwa hao wa nchi walitinga raundi ya kwanza wakitarajiwa kucheza na Platinum Fc ya Zimbabwe katika hatua hiyo
Mashabiki walitamani kumuona Kagere kwa muda mrefu kwenye mchezo huo kutokana na ukweli kuwa walinzi wa Plateau walimpa wakati mgumu nahodha John Bocco
Kagere ndiye kinara wa mabao katika michuano ya ligi ya mabingwa akiwa amefunga jumla ya mabao saba ndani ya kikosi cha Simba
Wanamsimbazi wanafahamu shughuli yake anapokuwa uwanjani, pengine ndio sababu kwa nini wengi wanahoji kulikoni Sven hamuamini?
Ili kufanikiwa kwenye michuano hii ya ligi ya mabingwa, kwa uzoefu wa michuano iliyopita, ushindi nyumbani ni matokeo muhimu sana
Wengi wanahofu huko mbeleni hasa kuanzia hatua ya makundi, kama timu haitashinda mechi za nyumbani inaweza isifanikiwe malengo yake
Kocha Sven Vandenbroeck amesema kila mchezo una mbinu zake, aliwasoma Plateau United na anaamini walipaswa kuwakabili kwa tahadhari na muhimu zaidi ni kuwa matokeo ya kuwavusha hatua ya awali wameyapata