Machampioni wa nchi hii Simba keshokutwa Jumamosi wana jambo lao hapo uwanja wa Benjamin Mkapa wakishuka dimbani kuikabili Plateau United katika mchezo wa ligi ya mabingwa, mchezo wa marudiano
Simba imeanza vyema michuano hiyo msimu huu kwa kupata ushindi muhimu wa bao 1-0 kule Nigeria. Wekundu wa Msimbazi wakiandika Historia kuwa timu pekee kutoka Tanzania iliyoweza kushinda nchini Nigeria
Sasa Jumamosi watakuwa na kazi moja tu, kusaka ushindi ili waweze kutinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo
Hesabu zote ni kwa Mnyama kushinda, lakini hata akipata matokeo ya sare atafuzu
Kinachowapa jeuri Wanamsimbazi ni kuwa wana kikosi imara sana. Lakini pia katika mechi za hivi karibuni, Simba imeweka rekodi nzuri ya kutofungwa nyumbani
Katika mechi saba zilizopita, Simba imeshinda mechi tano na kutoka sare mechi mbili
Miongoni mwa mechi walizoshinda ni pamoja na kuwafunga mabingwa wa sasa wa Afrika Al Ahly na klabu ya AS Vita
Hebu tujikumbushe matokeo ya michezo saba ya mwisho nyumbani;
Simba 4-0 Mbabane Swallows
Simba 3-1 Nkana
Simba 3-0 JS Soura
Simba 1-0 Al Ahly
Simba 2-1 AS Vita
Simba 0-0 TP Mazembe
Simba 1-1 UD Songo
Kwa mwenendo huo, ni wazi Plateau United watahitaji muujiza kuweza kuchomoka na alama zote tatu mbele ya Simba ambayo imerejea katika makali yake waliyokuwa nayo mwaka juzi katika michuano hiyo