Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck amewapongeza wachezaji kwa kufanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ys Plateau United ugenini nchini Nigeria katika mchezo wa hatua ya awali ligi ya mabingwa
Sven amesema wachezaji wake walipambana kuhakikisha wanapata matokeo hayo muhimu yanayowafanya wawe kifua mbele kuelekea mchezo wa marudiano ambao utapigwa jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki hii
Aidha Sven amesema, wanarejea kujipanga kwa ajili ya mchezo huo kwani wanafahamu bado wana dakika nyingine 90 za kupambana
"Ulikuwa mchezo mgumu, wana nguvu na walijaribu kiufundi kutafuta goli lakini nawapongeza wachezaji wangu sababu dakika zote 90 walikuwa wanakimbia kuzuia. Nafikiri tunatakiwa kuwa na furaha sana na ushindi. Matokeo mazuri lakini bado hatujamaliza sababu wiki ijayo tuna dakika 90 zingine," alisema Sven
Bao la dakika ya 53 lililofungwa na Mzambia Clatous Chama lilitosha kuwazamisha Plateau United katika ardhi yao licha ya figisu nyingi walizofanya kabla ya mchezo huo
Kimahesabu, kwenye mchezo wa marudiano, Simba itahitaji ushindi au matokeo yoyote ya sare iweze kutinga raundi ya kwanza
Lakini muhimu zaidi Simba itacheza mchezo huo ikiwa nyumbani, tena mbele ya mashabiki wake takribani 30,000 ambao wataruhusiwa kuingia uwanja wa Benjamin Mkapa