Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck amesema pamoja na kuwa mchezo wao wa kwanza dhidi ya Plateau United unapigwa ugenini, wanapaswa kupambana ikiwezekana wapate ushindi ambao utawaweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele raundi ya kwanza michuano ya ligi ya mabingwa
Simba itacheza na Plateau United Jumamosi mchezo wa kwanza ukipigwa Mji wa Jos ambao uko takribani kilomita 1000 kutoka Lagos
Sven amesema kwa uzoefu wake na soka la Afrika, wanapaswa kupata matokeo mahali popote bila ya kujali wako nyumbani au ugenini
Aidha amesema kama watashinda ugenini, itawaongezea kujiamini na watafanya vizuri zaidi katika mchezo wa pili utakaopigwa nchini
"Wachezaji wangu wanafahamu nini wanapaswa kufanya kwenye mchezo wetu wa kwanza ugenini. Hatuhitaji kuwa na presha katika mchezo wetu tutakaocheza nyumbani hivyo tunapaswa kupata matokeo Nigeria," alisema Sven mda mfupi kabla timu haijaondoka kuelekea Nigeria wakipitia Ethiopia
"Tuna malengo ya angalau kufika hatua ya makundi hivyo tunapaswa kuanza kushinda mchezo wa kwanza ili tuweze kusonga mbele hatua inayofuata"
Habari njema kwa Simba ni kuwa mchezo dhidi ya Plateau United utapigwa bila ya mashabiki kule Nigeria lakini mchezo wa marudiano utakaopigwa nchini wiki ijayo, mashabiki takribani 30,000 wataruhusiwa kuingia uwanja wa Benjamin Mkapa