Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck amesema wanapaswa kujiandaa kikamilifu kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa hatua ya awali dhidi ya Plateau United kutoka nchini Nigeria
Baada ya ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliopita kwenye ligi, matumaini ni makubwa kwa mashabiki wa Simba kuwa wanakwenda Nigeria kuendeleza moto huo wa ushindi
Hata hivyo Sven amesema ushindi huo usiwapumbaze kwani hii ni michuano miwili tofauti
"Kuna tahadhari tunapaswa kuchukua. Naona baada ya kushinda mabao 7-0 wengi wadhani itakuwa rahisi pia kwenye mchezo dhidi ya Plateau. Tunapaswa kufahamu tunakwenda kukabiliana na timu imara zaidi"
"Ulikuwa ushindi mzuri ambao umetuandaa vizuri lakini bado tunapaswa kuwa makini na tahadhari kuelekea mchezo wetu kule Nigeria," alisema Sven
Sven amesema wanaendelea na maandalizi kuelekea mchezo huo jana akiwapokea kambini Meddie Kagere na Luis Miquissone waliorejea kutoka kwenye majukumu ya timu za Taifa
Simba inatarajiwa kuondoka nchini siku chache zijazo kuelekea Nigeria tayari kwa mchezo huo wa kwanza utakaopigwa mwishoni mwa wiki