Baada ya ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha jana, kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba sasa kinahamishia nguvu zake kwenye michuano ya ligi ya mabingwa
Jumamosi ijayo, Simba itakuwa nchini Nigeria kuwakabili mabingwa wa nchi hiyo Plateau United
Ni mchezo wa kwanza wa hatua ya awali michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu. Timu hizo zitarudiana nchini baada ya wiki moja
Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck jana aliwapa mapumziko baadhi ya wachezaji wake muhimu Meddie Kagere, Jonas Mkude na Luis Miquissone hesabu zake zikiwa mechi ya Plateau
Wanasimba wana matumaini makubwa na klabu yao, hawatapenda kuona kile kilichojitokeza msimu uliopita kutokea tena msimu huu
Pamoja na kwenda kucheza ugenini, Simba inatakuwa na lengo la kushinda huko Nigeria. Matokeo mazuri ugenini yatarahisisha kazi kwenye mchezo wa nyumbani ambao utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bilionea Mohammed Dewji 'Mo' amesema ili kuepuka changamoto ya hujuma, wanakusudia kutumia ndege ya kukodi itakayowapeleka mpaka mji wa Jos ambao upo kilomita 1000 kutoka jiji la Lagos