Usiku wa kuamkia leo Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni Wanachama wa klabu ya Simba walishiriki hafla maalum ya kukaribishwa mkoani Dodoma hafla ambayo iliongozwa na Spika wa Bunge, Mwanasimba lialia Mh Job Ndugai
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bilionea Mohammed Dewji 'Mo' ndiye aliyekuwa mgeni rasmi akipata nafasi ya kuhutubia
Mo aliwahakikishia Wabunge kuwa klabu imejipanga kufikia malengo akiwataka wadau wote wa kSimba waunge mkono juhudi zinazofanywa na viongozi wao
"Malengo ya Simba yamegawanyika katika hatua tatu, malengo ya muda mfupi ni kuendelea kutetea ubingwa wetu. Malengo ya muda wa kati tunadhamiria kujenga klabu endelevu. Malengo ya muda mrefu ni Simba kushinda ubingwa wa Afrika," alisema Mo
"Simba ndio klabu ya kwanza Afrika ambao inakiongozi mwanamke Miss Barbara. Simba ndio timu ambayo inalipa vizuri kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na Simba ndio klabu ya kwanza kupata tuzo ya YouTube kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati."
"Tathmini inaonyesha kwamba Simba tupo nafasi ya tano kwa kufuatiliwa sana kwenye mitandao Afrika kwa vilabu. Simba tumekuwa kama maji usipotuoga utatunywa, ulipo tupo."
"Utafiti ambao umefanyika hivi karibuni unaonyesha kwamba Watanzania saba katika kila watu 10 ni mashabiki wa Simba."
"Mimi naamini mwisho wa safari ya mageuzi wale wanaotusema vibaya sasa watatupenda. Tumejipanga na tumedhamiria. Tunawaomba mtuunge mkono. Napenda kuwatoa hofu kuhusu Bilioni 20, hakuna haja ya kuwa na hofu. Simba kwangu sio biashara bali ni familia kwanza. Mapenzi yangu kwa Simba hayapimiki kwa fedha. Matamanio yangu ni Simba kufanikiwa kimataifa."
Miongoni mwa matukio aliyofanya Mo katika hafla hiyo ni kuwakabidhi zawadi ya jezi Spika wa Wabunge pamoja na wabunge wengine Wanasimba waliohudhuria hafla hiyo

