Mlinzi wa kulia wa Simba Shomari Kapombe amesema bado ana imani watatetea ubingwa wao kwa msimu wa nne mfululizo licha ya kuanza msimu taratibu
Juzi Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya watani zao Yanga katika mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Huo ulikuwa mchezo wa nne msimu huu Simba haijafanikiwa kushinda ikiwa imeshuka dimbani mara 10, imefungwa mechi mbili na kutoka sare mechi mbili
Kapombe amesema bado anaona Simba ndio timu yenye kikosi imara zaidi hivyo hakuna sababu kwao kushindwa kutwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo
"Najua tuna kazi kubwa mbele yetu, ili tuweze kufikia malengo yaliyowekwa mwanzoni mwa msimu tunapaswa kupambana"
"Lengo kuu ni kuhakikisha tunashinda ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo. Nadhani tunaweza kufanikisha hilo kwani kila mchezaji katika kikosi chetu ndio kiu yake," alisema Kapombe
"Tumedondosha pointi katika michezo ya hivi karibuni lakini ndivyo ilivyo wakati mwingine, tunachopaswa kufanya ni kusahau matokeo hayo na kujipanga kufanya vizuri katika michezo inayokuja mbele yetu"
"Tunawaomba mashabiki waendelee kutuunga mkono, kwani bila ya wao hatuwezi kufikia malengo, uwepo wao viwanjani unatuongezea ari na morali ya kupambana"
Simba itarejea dimbani baada ya mechi za timu za Taifa kuwania kufuzu fainali ya michuano ya Afcon 2021. Novemba 21 itasafiri jijini Tanga kuifuata Coastal Union kisha kuelekea mkoani Dodoma kuchuana na Dodoma Jiji Novemba 24