Kiungo wa Simba Clatous Chama amesema hayakuwa matarajio yao kulazimishwa sare na klabu ya Yanga lakini wataendelea kupamba kuhakikisha wanatimiza malengo yao
Licha ya kocha wa Simba Sven Vandenbroeck kutangaza kuwa Chama angekosa mchezo dhidi ya Yanga jana, Mwamba huyo wa Lusaka aliibuka uwanjani na kuwa sehemu ya kikosi kilichopambana na kulazmishwa sare ya bao 1-1
"Alama moja mwisho wa siku, hatukuridha na matokeo haya lakini mapambano lazima yaendelee. Tutaendelea kupambana kuhakikisha tunapata kile ambacho ni haki yetu," aliandika Chama kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii
Mashabiki wamtetea Chama
Katika hatua nyingine mashabiki wa klabu ya Simba wameonesha kukerwa na kauli ya Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Zacharia Hanspoppe kuwatuhumu baadhi ya wachezaji kuwa huenda wlaitumika jana kuihujumu Simba
Hanspoppe aliwatuhumu Chama, Larry Bwalya na Luis Miquissone kuwa hawakuwa katika viwango vyao na uongozi utawahoji kubaini nini kiliwakumba katika mchezo huo
Wanasimba katika mitandao ya kijamii wamepinga kauli hiyo ya Hanspoppe na kuwa haikupaswa kutolewa na kiongozi wa kariba yake tena katika media
"Siku hazifanani kuna wakati tunapaswa kukubaliana na matokeo. Si jambo jema kwa kiongozi kuwalaumu wachezaji hadharani kwa mambo ambayo hayapo. Unamtuhumu mchezaji kuwa amehujumu timu kwa kukosa bao? Mbona kina Ronaldo, Messi nao hukosa mabao ya wazi?"
"Viongozi wetu waache mihemko ya kishabiki, kama lipo tatizo wanapaswa wazungumze ndani na sio mbele ya Wanahabari, matamshi yake yanaweza kuwafanya wachezaji wakahisi kama mchango wao hauthaminiwi"
"Chama na Miquissone ni wachezaji wanaojitolea sana Simba, siamini kama wanaweza kufanya hujuma, kilichotokea ni sehemu ya matokeo ya mpira wa miguu," alisema Mwanamsimbazi aliyejitambulisha kwa jina moja la Rashid