Kocha Mkuu wa mabingwa watetezi ligi kuu ya Vodacom, Simba, Sven Vandenbroeck amesema watafanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika mechi zilizopita ili kuweza kupata matokeo chanya mechi zinazofuata.
Mbelgiji huyo Jumamosi atakiongoza kikosi chake mchezo dhidi ya Mwadui FC , mchezo ambao unaweza kumuweka matatani kama atakosa ushindi
Kikosi cha Sven kimepoteza alama sita mfululizo kwa kufungwa na Tanzania Prisons na Ruvu Shooting.
Sven amesema hajui sababu kwa nini timu yake ilipoteza mechi hizo lakini anaamini ni nyakati tu zinazopita anaamini kwamba watafanya vizuri mechi zijazo.
"Sikumbuki mara ya mwisho kupoteza mechi mbili nikiwa Kocha Mkuu ilikuwa lini ila mpaka sasa ninaona kwamba haya kwangu ni maajabu kutokea.
"Kwa kuwa mchezo wa mpira ni makosa, basi kwa yaliyotokea tunayafanyia kazi na kuona kwamba tutarekebisha kwenye mechi zetu zijazo," alisema Sven