Pamoja na ubora wake alioonyesha kwa takribani misimu minne, Aishi Manula mlinda lango namba moja wa Simba amekuwa akisumbuliwa sana na mipira ya krosi pamoja na mipira inayopigwa mbali
Hili la mipira ya mbali anaweza kusamehewa kwani hiyo ni changamoto ya makipa wengi kote duniani
Lakini hili la maamuzi katika utokeaji wa mipira ya krosi, benchi la ufundi la Simba linapaswa kumsaidia ili aepuke kufungwa mabao yaleyale kila mara na kuingizwa kwenye lawama za mashabiki
Bao alilofungwa katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar halina tofauti na bao alilofungwa katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons
Ukiangalia hata msimu uliopita, Simba iliruhusu mabao mengi kupitia mipira ya krosi
Baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, kocha mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck alisema hawezi kumlaumu mchezaji yeyote kwani wachezaji wote walicheza vile walivyopaswa
Hata hivyo aliahidi kuwa watafanyia kazi maeneo yote yaliyoonekana kuwa na mapungufu ili kuhakikisha wanashinda mchezo wa Jumatatu dhidi ya Ruvu Shooting
Baadhi ya mashabiki wa Simba wamehoji kwa nini mlinda lango namba mbili Beno Kakolanya hapewi nafasi
Pengine kesho anaweza kuanza langoni ili kumpa changamoto Manula ambaye msimu huu amecheza mechi zote za Simba