Inaelezwa mshambuliaji Meddie Kagere amepata majeraha ambayo yanaweza kumuweka nje kwa wiki tatu
Mfungaji bora huyo kwa misimu miwili mfululizo aliumia kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania ambao ulipigwa mkoani Dodoma Simba ikiondoka na ushindi wa mabao 4-0
Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema Kagere ameongeza idadi ya majeruhi kikosi cha Simba lakini wana matumaini ataweza kurejea haraka
"Tunao wachezaji majeruhi, Gerson Fraga ambaye anaendelea vizuri, John Bocco ameshaanza mazoezi mepesi. Mwingine ni Meddie Kagere ambaye kwa mujibu wa jopo la madaktari atakaa nje kwa takribani wiki tatu mpaka pale hali yake itakapotengemaa, atarejea uwanjani.
"Matarajio yetu Wanasimba wataendelea kuwaombea wachezaji wetu ambao wamepata majeraha kwa ajili ya kuitumikia timu hii," alisema Manara
Simba iko nyanda za juu Kusini ambapo keshokutwa Alhamisi inakabiliwa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons
Kinara wa mabao kwenye kikosi cha Simba msimu huu Chris Mugalu anatarajiwa kuongoza mashambulizi dhidi ya Prisons
Lakini pia Charles Ilanfya ni miongoni mwa washambuliaji ambao wako mkoani Mbeya na kikosi cha Simba