Baada ya ushindi wa mabao 3-1 hapo jana dhidi ya Mlandege Fc kwenye mchezo wa kirafiki, mabingwa wa nchi Simba wanatarajiwa kuendelea na mazoezi leo yakiwa ni maandalizi ya mwisho kabla ya safari ya Sumbawanga kuwafuata Tanzania Prisons kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu utakaopigwa Alhamisi, Oktoba 22
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, amesema kikosi chao kitaendelea na mazoezi yake leo asubuhi na maandalizi ya safari ya kuelekea Sumbawanga kuwafuata Tanzania Prisons yamekamilika.
Rweyemamu alisema wataondoka na wachezaji wote ambao wako tayari kwa mechi hiyo, huku majeruhi wakiendelea na programu maalumu za mazoezi chini ya mwongozo wa daktari wao, Yasin Gembe.
Alisema Tanzania Prisons ni moja ya timu zenye vikosi imara na kupata matokeo mazuri inatakiwa kujipanga na kuongeza umakini.
"Tutaondoka Jumatatu na kwenda kupumzika Mbeya, kesho yake (Jumanne), ndio safari ya kwenda Sumbawanga itaanza, tunajua huko tunakwenda kukutana na timu inayotoa changamoto, hatutabweteka, ni mechi itakayokuwa na ushindani," Rweyemamu alisema.
Aliongeza ushindani katika kikosi cha Simba unaongezeka kila siku kwa sababu kila mchezaji anahitaji kuwa sehemu ya wachezaji 18 ambao Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck anawaamini kuelekea mchezo husika.
Aliwataka mashabiki na wanachama wa Simba kuendelea kushirikiana na viongozi ili kufikia malengo ya timu kwa sababu msimu huu ni mgumu zaidi.
"Kuchukua ubingwa wa ligi mara tatu mfululizo si jambo dogo, timu zote 17 zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara zinatuangalia sisi, sio kwa sababu tuna kikosi kizuri, zinataka kutupa changamoto mabingwa watetezi, tunalijua hilo, tumejipanga vizuri kutetea taji," alisema meneja huyo.