Washambuliaji Chris Mugalu na Meddie Kagere wamempa jeuri kocha mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck akiwa na uhakika wa kuendelea kufanya vizuri ndani ya Ligi Kuu Bara na hata wakianza kucheza mechi za kimataifa.
Sven amesema kuwa wachezaji wake hao pamoja na wengine wanaocheza eneo la ushambuliaji akiwemo Bernard Morrison wanampa uhakika wa kushinda kwenye mechi yoyote ile kwani nje ya kufunga wanajua kutengeneza nafasi.
Mugalu na Kagere wote kwa sasa wamefunga mabao mawili kwenye ligi wakiwa sawa na kiungo Mzambia Clatous Chama na Mzamiru Yassin.

Sven amesema kuwa uwezo huo wa juu wa kufunga wa mastraika wake hao unampa mwanga wa kuona ana uwezo wa kushinda mechi yoyote bila ya kujalisha ni ya ligi au ya kimataifa.
"Tuna washambuliaji wengi wazuri ambao wanajua kwa kiasi kikubwa kufunga, kitu ambacho ni kizuri kwangu kwa sababu hatutegemei mtu mmoja kwenye hilo.
"Wanacheza kitimu na kupeana nafasi ambazo zinatufanya tuwe na uhakika wa kushinda kwenye mechi yoyote ile iwe ya ligi au kimataifa ambapo tuna miezi michache kabla ya kuanza kupambana," alimaliza Sven