Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Haji Manara amewataka mashabiki wa timu hiyo kutoyumbishwa na tetesi za mitaani kuhusu mchezaji wao bora zaidi nchini Clatous Chama
Hivi karibuni zimeibuka tetesi nyingine katika mitandao ya kijamii kuhusu hatma ya fundi huyo wa mpira ambaye mkataba wake unamalizika Julai 2021
Baada ya mchezo dhidi ya Biashara United, kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck alieleza kuwa na hofu ya kumpoteza Chama kama hataongezwa mkataba sasa kutokana na kiwango cha juu alichonacho
Sven alisema Simba haipaswi kusubiri mkataba wake umalizike ndio apewe mwingine kwani huenda kutakuwa na ushindani kutoka timu nyingine ambazo tayari zimeonyesha nia ya kutaka huduma yake

Akiwa katika ziara ya kutembelea vyombo vya habari, Manara alisema uongozi wa Simba unafahamu umuhimu wa Chama hivyo hawatamruhusu aondoke
Amesema hakuna haja ya kuyumbishwa na tetesi hizo, ukiachilia mbali mazungumzo ya mkataba mpya, Chama bado ana zaidi ya miezi kuendelea kuitumikia Simba
"Chama bado ana mkataba na Simba mpaka mwezi Julai 2021. Mashabiki wasibabaishwe na propaganda za mitandaoni, viongozi wana uchungu na Timu hawawezi kuruhusu Clatous Chama aondoke," alisema Manara
Tangu kuanza msimu huu Chama ameonesha kiwango cha juu sana, ni wazi kutakuwa na ushindani mkali kumbakisha kama hataongezewa mkataba mpaka mwakani