Uongozi wa klabu ya Simba umekanusha taarifa kuwa jana asubuhi ilicheza mechi ya kirafiki na Green Warriors na kulala kwa mabao 2-1.
Kupitia kipindi cha michezo cha Sports Extra kinachorushwa na Clouds FM kilitoa taarifa kuwa mabingwa hao wamecheza mechi hiyo na kupoteza kwa mabao 2-1 kitu ambacho Simba wenyewe wamekanusha.
Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara amesema kikosi chao jana asubuhi kilikuwa na ratiba ya Gym na jioni kikafanya mazoezi katika viwanja vyao vya Mo Simba Arena hivyo taarifa hiyo nia yao ni kuwatoa mchezoni kuelekea mechi yao ya Jumapili.
"Hatukucheza mechi yoyote jana, tulikuwa na ratiba ya Gym asubuhi na jioni mazoezi lakini kuna watu wanataka kututoa kwenye reli kuelekea mchezo wetu wa Jumapili. Wanasimba wenzangu msichanganyikiwe kikosi kipo kamili kuelekea mechi yetu dhidi ya Biashara United," amesema Manara.