Mkufunzi wa Simba, Sven Vandenbroeck huenda akakifanyia mabadiliko kikosi chake kitakachoikabili Biashara United siku ya Jumapili kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Katika mazoezi yanaendelea uwanja Mo Simba Arena, Sven amekuwa akiwatumia mshambuliaji Chris Mugalu na kiungo fundi Larry Bwalya katika kikosi chake cha kwanza
Mbelgiji huyo ni kama anaangalia uwezekano wa kuwajumuisha wachezaji hao kwenye timu yake
Nyota hao waliotua kutoka Lusaka Dynamos ya Zambia, bado hawajajihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza, mashabiki wana shauku ya kuwaona wakitumika


Kwa mara ya kwanza wote walipata nafasi kwenye mchezo wa Simba Day dhidi ya Vital'o Bwalya akionyesha kiwango cha hali ya juu huku Mugalu akiwa mmoja wa wafungaji wa mabao ya Simba katika ushindi wa mabao 6-0
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema Sven ameahidi kuwapa furaha mashabiki wake baada ya kukosa ushindi mbele ya Mtibwa, hivyo atawapa nafasi wachezaji wengi ambao alishindwa kuwatumia mikoani kutokana na ubovu wa viwanja
“Uwanja ni mzuri baada ya kupambana na viwanja vya mikoani ambavyo siyo rafiki sana. Hapa Dar tutacheza soka letu na watu watafurahi kwa kuwa wachezaji wote mafundi wanaweza wakaanza kwenye mchezo huo,” alisema Rweyemamu