Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck amesema baada ya kuambulia alama moja kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, sasa wanaelekeza nguvu kwa mchezo unaofuata dhidi ya Biashara United ambao utapigwa Jumapili ijayo Septemba 20 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa
Aidha Mbelgiji huyo amewataka Wanamsimbazi wasiumizwe na matokeo ya mchezo uliopita, kwani bado ni mapema sana
Sven amesema wanapaswa kupokea matokeo ya mchezo uliopita kama changamoto ya kujipanga kwa mchezo ujao, ambao utakuwa fainali ya kusaka ushindi utakao warudisha kwenye mstari.
"Hii ni ligi bado tuna mechi nyingi mbeleni, sio wakati wa kukaa na kujuta tulichopata ila tumepokea kama changamoto kuona tunatengeneza mbinu mpya kujipanga na mechi ijayo dhidi ya Biashara," alisema Sven
Sven amebainisha kuwa msimu unapoanza kila timu inakuwa na lengo la kufanya vema kutengeneza msingi wa saikolojia ya ushindi kujipanga na mechi zilizo mbele yao, hivyo wao kama mabingwa watetezi bado wanatakiwa kuendelea kujipanga.
Lakini pia Sven amegusia kuhusu changamoto ya uwanja kuwa ni sababu iliyochangia kikosi chake kupata matokeo hayo, ambayo sio mabaya, lakini yanawapa picha ya kujipanga kiushindani kwenye kila mchezo unaokuja ili kupata ushindi na kutimiza malengo waliyojiwekea.