Mshauri wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi klabu ya Simba, Crescentius Magori amesema mchakato wa Uwekezaji uko katika hatua za mwisho kukamilika na wachosubiri ni kukamilishwa kwa baadhi ya nyaraka
Akihojiwa na redio moja maarufu mapema leo, Magori amesema pamoja na changamoto hiyo, Mwekezaji Mohammed Dewji 'Mo' ameendelea kujitolea kugharamia uendeshaji wa klabu
"Kuna nyaraka bado hazijakamilika ndizo zinazokwamisha kukamilika kwa mfumo mpya wa uwekezaji ndani ya Simba sc na kuhusu hizi bilion 2 za kila msimu Mo Dewji amekuwa akijitolea tu, "amesema Magori
Mapema wiki hii Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangala ambaye ni Mwanachama wa klabu ya Simba aliibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii akihoji utaratibu uliotumika kumteua Mwanamama Barbara Gonzalez kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba akidai kuwa Mwanamama huyo kabla alikuwa Msaidizi wa Mo
Pia akahoji kwa nini fedha za ununuzi wa hisa asilimia 49, Bil 20 bado Mwekezaji hajaziweka kwenye akaunti?
Mara kadhaa uongozi wa Simba umetolea ufafanuzi jambo hilo na Mo ameendelea kutimiza majukumu yake ya Uwekezaji ndani ya klabu ya Simba kwa mapenzi yake licha ya kuwa mchakato bado haujakamilka
Mafanikio iliyopata Simba katika misimu yake mitatu ni kielelezo cha kazi kubwa anayofanya Mo kwa kushirikiana na wadau wengine wa klabu ya Simba