Meneja wa klabu ya Simba Patrick Rweyemamu ameeleza kushangazwa na taarifa zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii zinazodai kuwa mshambuliaji Meddie Kagere alipigana na kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck
Akihojiwa na Redio Wasafi mapema leo, Rweyemamu alisema hakuna tukio la aina hiyo ambalo limetokea katika kambi ya Simba
Aidha amesema Kagere pamoja na kocha hawana tatizo lolote, wako mkoani Mbeya na kikosi cha mabingwa hao wa nchi ambacho Jumapili kitaanza kutetea ubingwa wake wa ligi kuu kwa kuumana na Ihefu Fc
Manara awashukia Wasafi FM
Katika hatua nyingine Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Haji Manara, amewataka Wanahabari kuacha kukuza masuala ya kwenye mitandao ya kijamii ambayo yanatolewa kizushi kwa lengo la kutaka kuvuruga utulivu ulio ndani ya Simba
Manara hakufurahishwa na Wasafi FM kufanya mjadala wa jambo ambalo Meneja wa Simba aliwathibitishia kuwa halipo
"Hamtutendei haki Simba kwa kujadili masuala ya kizushi ambayo hayapo. Sisi tumeshatoka huko siku nyingi sana. Hakuna mchezaji yeyote wa Simba ambaye anaweza kufanya jambo la kipuuzi kama hilo, tuko mbali sana, sasa tunawaza kutwaa ubingwa wa Afrika nyie mnaleta habari za mchezaji kupigana na kocha?"
"Redio yenu imejijengea heshima miongoni mwa mashabiki wa soka nchini lakini mnajishushia hadhi kwa kujadili masuala ya kizushi kutoka mitandaoni," alin'gaka Manara
Uongozi wa Simba umesisitiza kuwa hakuna tukio la kocha Sven vandenbroeck kupigana na Kagere, aidha, habari hiyo imewashangaza wengi kwani haina ukweli wowote