Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck amesema anaamini watakuwa na msimu mwingine mzuri kama nyota wake wataendeleza makali waliyoanza nayo
Jana Simba ilifanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa msimu wa nne mfululizo baada ya kuichapa Namungo Fc mabao 2-0
Bernard Morrison aliyechomolewa kutoka Yanga ndiye aliyekuwa habari ya mjini kwani alisababisha bao huku akifunga jingine
Akizungumza baada ya mchezo huo uliopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Sven alisema vijana wake walikuwa bora kwa muda mwingi, walistahili kuondoka na ushindi huo
"Nadhani kila mmoja ameona tumecheza vizuri. Tulishambulia kwa pamoja na hata kuzuia tulishirikiana vizuri. Nawapongeza Namungo, sio timu mbaya lakini nadhani tulistahili kushinda," alisema sven
"Bado tuna safari ndefu msimu huu, natarajia ushindani kuwa mkubwa kuliko msimu uliopita. Sasa timu zimepungua hivyo kila timu itakuwa na muda wa kutosha kujipanga kutoka mechi moja kwenda nyingine. Lakini timu zimefanya usajili mzuri, hivyo haitakuwa kazi rahisi"
"Tumeanza vizuri, vijana wako tayari kwa mapambano, kama tutaendelea kucheza hivi nadhani tutakuwa na msimu mzuri sio kwenye ligi tu, hata katika michuano mingine tutakayoshiriki"
Simba itaanza kampeni ya kutetea ubingwa kwa msimu wa nne mkoani Mbeya siku ya Jumamosi watakaocheza na vijana waliopanda daraja, Ihefu Fc katika uwanja wa Sokoine