Baada ya kumalizika kwa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2019/2020, klabu ya Simba imejinasibu kuanza maandalizi ya kujipanga na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kauli hiyo ilitolewa juzi mara baada ya kikosi hicho kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa kufunga pazia uliofanyika Uwanja wa Ushirika Moshi na Ofisa Mtendaji wa Simba, Senzo Masingiza alisema hawawezi kubweteka kwa sababu ligi imeisha, hivyo wanaanza maadalizi kwa mechi za kimataifa.
"Tumefanya vizuri kwenye Ligi ya ndani sasa tunayo dhamana ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa, hatuwezi kuwa bora kama hatutaanza maandalizi ya kujipanga mapema,"alieleza Masingiza.
Senzo alisema mipango ya kufanya usajili bado iko palepale ya kuleta nyota watakaokuja kuongeza nguvu, lakini hilo haliwezi kufanyika kipindi cha dirisha kubwa bila kufikiria wachezaji wakuwaacha kwakuwa wachezaji walipo walitoa huduma nzuri.
"Wachezaji wote walionesha ubora mkubwa wa kuitumikia timu, sasa tunapoingia kwenye usajili bado tuna kazi ngumu ya kuangalia tuwaache wachazaji gani kuwapisha wengine wapya, " alisema Masingiza
Pia Masingiza alisema bado wana kibarua kikubwa cha kumalizia mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Namungo FC, utakaofanyika Agosti 2,2020 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.
Alisema mara baada ya mchezo huo wa FA wataweka wazi mipango yao ya usajili kuhusu wachezaji gani wanawaacha na wale watakaosajiliwa kuelekea michuano ya kimataifa.