Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh Dkt. John Magufuli, ametangaza rasmi uwanja wa Taifa Jijini Dar Es Salaam, kuanzia leo, Julai 28, 2020, kuitwa Uwanja wa Taifa wa Mkapa (Mkapa National Stadium).
Rais Magufuli ameyasema hayo leo katika hotuba yake wakati wa kuhitimisha zoezi la kuuaga mwili wa Rais Mstaafu Awamu ya Tatu, Mh Benjamini William Mkapa aliyefariki wiki iliyopita
Rais Magufuli amesema amepokea maombi mengi ya watu, wakitaka Uwanja wa Taifa uitwe Uwanja wa Mkapa, ili kumuenzi Mzee Mkapa, hivyo ameridhia maombi hayo
Miongoni mwa waliotoa mapendekezo ya kuomba mabadiliko ya jina la uwanja huo ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi klabu ya Simba Mohammed Dewji 'Mo' ambaye alianzisha kampeni maalum kwenye mitandao ya kijamii akiwataka Watanzania kuweka sahihi maombi aliyopanga kumpelekea Mh Rais ili kubadili jina la uwanja huo ambao ulijengwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa chini ya Mzee Mkapa