Pamoja na timu yake kupata sare ya bila kufungana dhidi ya wenyeji Coastal Union juzi, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema alifurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake na kuongeza ni maandalizi mazuri kuelekea mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Namungo FC .
Kabla ya mchezo huo wa fainali, mabingwa Simba watashuka dimbani kesho Jumapili kufunga pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi.
Sven amesema watautumia mchezo huo kukamilisha maandalizi ya mechi ya Namungo ambayo itapigwa August 02, mkoani Rukwa
Mbelgiji huyo amesema mchezo wa Coastal Union ulikuwa na ushindani mkali na umewasaidia kujiimarisha, lengo lao ni kuhakikisha wanaendelea kucheza katika kiwango cha juu kesho na hatimaye kumaliza msimu kwa furaha.
"Ilikuwa mechi yenye ushindani kutoka kila upande, ingawa tulistahili ushindi, natumaini tutakuwa katika kiwango bora zaidi Jumapili na baadaye kwenye fainali ya FA, " alisema Sven
Simba tayari iko Wilayani Moshi ikiendelea na maandalizi ya kuikabili Polisi Tanzania, katika mchezo ambao utahitimisha safari ya msimu huu ambao tayari Simba imetwaa ubingwa