Tangu ligi iliporejea baada ya mapumziko ya Corona, mshambuliaji wa Simba Mnyarwanda Meddie Kagere alikabiliwa na ukame wa mabao, wakati mwingine akikosa nafasi ya kuanza mbele ya nahodha John Bocco
Hata hivyo Mnyarwanda huyo ni kama amezaliwa upya baada ya kupachika mabao matatu katika michezo miwili iliyopita
Mabao hayo yamemfanya aongeze idadi ya mabao yake aliyofunga msimu huu akifikisha mabao 22 na kuzidi kutimua vumbi kuelekea kiatu cha ufungaji bora kwa msimu wa pili mfululizo
Kagere anahitaji kufunga bao moja tu katika michezo miwili iliyobaki dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania ili kufikia rekodi yake ya mabao 23 aliyoweka msimu uliopita
Hakuna shaka, kama kocha Sven Vandenbroeck atampa nafasi katika michezo hiyo, anaweza kuifikia rekodi hiyo na pengine kuivunja
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Alliance Fc ambao alifunga mabao mawili, Kagere alisema amefarijika kufunga mabao hayo lakini furaha kubwa zaidi ni kufanikiwa kuisaidia Simba kutetea ubingwa wake kwa msimu wa tatu mfululizo