Jana Mabingwa wa nchi Simba waliwashushia Alliance Fc dozi ya mabao 5-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Luis Miquissone akipiga bao la aina yake, likitajwa kufanana na yale anayofunga mkali wa Barcelona, Lionel Messi.
Mbali ya Luis aliyecheka na nyavu dakika ya 64, wengine walioifungia Simba ni Meddie Kagere aliyepiga mawili dakika za 23 na 44, Deo Kanda dakika ya 75 na Said Ndemla dakika ya 86.
Bao la kufutia machozi la Alliance lilifungwa na Martin Kigi dakika ya 38 ya mchezo huo.
Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa mabingwa Simba tangu walipotwaa taji la ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu Juni 29, baada ya kutoka suluhu na Tanzania Prison katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Simba sasa imefikisha pointi 84 baada ya kucheza michezo 36, ikishinda 26, sare sita na kupoteza minne.
Tayari wameshasherehekea ubingwa, sasa wakijiandaa na mchezo wa fainali ya kombe la FA dhidi ya Namungo Fc ambao utapigwa August 02 huko Sumbawanga mkoani Rukwa
Miquissone amekuwa akionyesha uwezo wa hali ya juu tangu aliposajiliwa na Simba mwezi January akitokea klabu ya UD Songo aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo akitokea klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini
Miquissone amekuwa gumzo kwa mashabiki wa soka nchini kutokana na uwezo wake