Msimu unaelekea ukingoni na tayari Simba imeweza kutwaa ubingwa wa ligi kuu kwa msimu wa tatu mfululizo
Mabingwa hao wa nchi wamebaki na deni moja tu, taji la FA ili kumaliza msimu wakiwa na mataji mawili
Kwa soka linalochezwa na Simba msimu huu unaomalizika, ni rahisi sana kusema kwa soka la Tanzania Simba haina mpinzani hivyo hata kwa maandalizi yake ya msimu ujao lazima yaangalie Kimataifa
Ni kwa sababu michuano ya ligi ya mabingwa ina ushindani mkubwa sana, hivi vitimu vyetu vya hapa Bongo hakiwezi kuwa kipimo sahihi cha kufanya vizuri kwenye michuano hiyo
Na ndio maana tayari maoni yameanza kutolewa na wadau wakitaka kuona Simba inatumia dirisha la usajili kuboresha maeneo yote yenye mapungufu na hata wapo wanaotaka kuona mabadiliko ya benchi la ufundi
Ndio, hilo limekuwa kizingumzwa katika viunga vya Wanamsimbazi na taarifa za karibuni zimebainisha kuwa mabadiliko ya benchi la ufundi yanaweza kutokea kama pendekezo litapitishwa na Bodi ya Wakurugenzi baada ya msimu kumalizika
Anayetajwa sana ni kocha wa AS Vita Florente Ibenge ambaye kwa takribani misimu mitano mfululizo, ameshiriki michuano ya ligi ya mabingwa na kombe la Shirikisho akiwa na AS Vita na kucheza hatua ya makundi kwake ni jambo la kawaida

Kocha Mkuu wa sasa wa Simba Sven Vandenbroeck nae anaweza kuongezewa mkataba pia kutegemeana na mapendekezo ya mabosi wa Simba
Hata hivyo wapo wasio na imani kama ataweza kuipa mafanikio Simba kwenye michuano ya ligi ya mabingwa
Zipo hoja zinazodai kufanikiwa kwake Simba kumetokana na ubora wa kikosi na sio ufundi wake
Lakini pia alikabidhiwa mikoba ya Patrick Aussems ambaye alikuwa tayari ameiweka timu katika mazingira salama
Kwako mdau Mwanamsimbazi unadhani kipi kifanyike, tuendelee na Vandenbroeck au Mo atuletee Ibenge?