Wakati wakisalia na michezo mitatu kumaliza msimu huu wa 2019/20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mabingwa wa ligi hiyo, Simba wamesema wataendelea kujiimarisha ili kuchukua kikombe cha mashindano ya Kombe la FA
Simba itavaana na Namungo FC katika mechi ya fainali ya Kombe la FA, itakayochezwa Agosti 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela ulioko Sumbawanga mkoani, Rukwa.
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola amesema wanahitaji kukamilisha msimu kwa kutwaa kikombe hicho na hawataingia uwanjani kuikabili Namungo kinyonge.
Matola alisema kila mchezaji wa Simba amejiandaa kuonyesha kiwango cha juu katika mchezo huo ambao utakuwa wa mwisho msimu huu.
"Tunajua hakuna mechi rahisi, kila mechi kwetu ni sawa na fainali, na huko Rukwa tutakwenda katika kukamilisha msimu, tunajipanga kumaliza msimu kama tulivyouanza, lakini pia tunatakiwa kushinda mechi za ligi zilizobakia," alisema Matola
Simba ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa tatu mfululizo, ilianza msimu huu kwa kunyakua Ngao ya Jamii kwa kuifunga Azam FC mabao 4-2