Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba wametinga kibabe nusu fainali ya michuano ya kombe la FA (ASFC) baada ya kuichapa Azam Fc mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa
Simba imeshinda mchezo huo huku ikionyesha kandanda ya hali ya juu wakiwaacha Azam Fc wasijue la kufanya
Nahodha John Bocco ndiye aliyeitanguliza Simba kwa bao safi kwenye dakika ya 40 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Francis Kahata
Ulikuwa mchezo ambao nyota wa Simba walifanya kila watakavyo, ni moja ya mechi bora ambazo Simba imecheza msimu huu
Bao la pili liliwekwa kambani na fundi Clatous Chama kwenye dakika ya 57 akiweka kambani mpira kwa shuti la chinichini baada ya gonga gonga za hapa na pale
Mabao yangekuwa mengi zaidi kama washambuliaji wa Simba hasa Luis Miquissone alipata nafasi kadhaa ambazo hakuweza kuzitumia
Ushindi huo unazikutanisha tena Simba na Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali
Hakika huo utakuwa mchezo wa kisasi kwa Simba
Mapema Sahare All Stars iliweka rekodi ya kuwa timu pekee ya ligi daraja la kwanza kutinga nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuitoa Ndanda Fc kwa mikwaju ya penati
Ni baada ya matokeo ya sare ya bao 1-1 kwenye mchezo ambao ulipigwa uwanja wa Mkwakwani, Sahare ikishinda kwa mikwaju 4-3