Ukiiondoa Simba ambao tayari ni mabingwa wa nchi kwa msimu wa tatu mfululizo, Azam Fc ndio klabu ambayo inatizamwa kushika namba mbili kwa ubora msimu huu
Hawa Azam Fc tayari wamekutana na Simba mara tatu msimu huu, licha ya kufungwa mechi zote tatu, lakini walitoa upinzani na kuonyesha kandanda safi mbele ya mabingwa hao wa nchi
Timu hizo leo zinakutana kwa mara ya nne huku kila timu ikiwa na malengo tofauti
Simba wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa hawana presha kwani tayari ni mabingwa wa ligi kuu, mkononi wanayo tiketi ya kucheza michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao
Lakini kutwaa ubingwa wa FA pia ni moja ya malengo ambayo Simba imejiwekea. Na pia ikumbukwe ushindi katika mchezo wa leo, utaihakikishia Simba kuwa na nafasi nyingine ya kukutana na watani zao Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali
Hivyo ni mchezo ambao wachezaji wanafahamu ushindi utawakutanisha na Yanga, mechi ya nusu fanali ambayo itakuwa ya kisasi kwa Simba
Kwa upande wa Azam Fc wao wanalihitaji sana taji la FA kwani ndio nafasi pekee itakayowahakikishia kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao
Hivyo kwao hii ni kama mechi ya fainali, wanafahamu kama watatoboa mbele ya Simba, watakuwa na matumaini ya kuhifadhi taji lao kwa msimu wa pili
Yanga sio timu ambayo inaweza kuwasumbua kama watakutana nayo kwenye nusu fainali
Mazingira haya yanaufanya mchezo wa leo kuwa na mvuto wa kipekee na kwa hakika mashabiki watapata burudani ya kutosha kutoka kwa miamba hawa
Muda wa mchezo ulibadilishwa kutoka saa kumi jioni kupelekwa saa moja usiku