Kiungo 'mgumu' raia wa Brazil Gerson Santos Fraga amekuwa kwenye kiwango bora mechi mbili zilizopita, akiwapa raha mashabiki na kuwafunga kabisa midomo wale waliokuwa wakimuandama kwa maneno
Nyota huyo ambaye yuko ukingoni mwa mkataba wake, amejiwekea mazingira mazuri ya kuramba mkataba mpya kwa mabingwa hao wa ligi kuu misimu mitatu mfululizo
Fraga ameeleza kufurahishwa na shangwe za mashabiki kila wanapomuona dimbani, akieleza kuwa ni chachu kwake kufanya vizuri pamoja na timu kwa ujumla
"Mimi kama mchezaji kazi yangu ni kuhakikisha naisaidia timu kushinda kila mchezo ambao nitapata nafasi ya kucheza. Lengo langu nikuisaidia Simba kutwaa ubingwa na kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika mwakani," Fraga aliiambia tivuti ya Simba Sc
"Nawaomba mashabiki wetu kuendelea kutusapoti katika mechi yetu iliyobaki ili tufanikishe kuchukua ubingwa"
Pasipo na shaka, Fraga anatarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha Simba siku ya kesho ambacho kinaweza kukamilisha mbio za ubingwa msimu huu kwa ushindi au hata matokeo ya sare dhidi ya Tanzania Prisons