Kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui Fc juzi, benchi la ufundi la Simba limesema harakati za kutangaza ubingwa kwao zinaanzia mkoani Mbeya baada ya matokeo ya sare ya mchezo kati ya Yanga dhidi ya Azam Fc ambao ulipigwa jana uwanja wa Taifa
Simba juzi ilifikisha pointi 75 baada ya kuifunga Mwadui, ukiwa ni mchezo wao wa 30, hivyo kuhitaji pointi nane tu kutoka katika mechi zao nane zilizobaki kutangaza ubingwa.
Pointi hizo zitaiwezesha Simba kufikisha pointi 83 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote Ligi Kuu Tanzania Bara, si Azam itakayotimiza pointi 82 wala Yanga watakaokusanya pointi 80 iwapo watashinda michezo yao yote iliyobaki.
Kocha Msaidizi wa Simba Selemani Matola amesema baada ya Yanga na Azam kusuluhu, sasa safari ya kutangaza ubingwa wanaianzia Mbeya pale watakapocheza mechi mbili na kuvuna alama sita.
"Tunakwenda Mbeya kucheza mechi mbili ambazo tunahitaji ushindi ili kupata alama sita zitakazotufikisha pointi 81, pengine tutahitaji alama nyingine mbili ambazo tunaweza kuzipata Mtwara tutakapokwenda kucheza na Ndanda"
Hata hivyo Matola amesema ni lazima wachezaji wapambane na kupata matokeo ya alama tatu ambazo zitatimiza wanachohitaji.
“Kama wachezaji watafanya makosa yoyote yatakayosababisha tupoteze mchezo, yatatuongezea safari na kuifanya iwe ngumu, hivyo lazima hili suala litimie mapema sana"
Kikosi cha Simba tayari kiko mkoani Mbeya ambapo leo jioni wameanza maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Mbeya City ambao utapigwa Jumatano