Baada ya kudondosha alama mbili kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting, kikosi cha Simba kimepania kuondoka na alama zote tatu katika mchezo unaofuata dhidi ya Mwadui Fc
Mchezo huo ambao utapigwa Jumamosi, Juni 20 kwenye uwanja wa Taifa, utakuwa wa kisasi kwa Simba kwani katika mchezo wa kwanza uliopigwa mkoani Sihinyanga, Mwadui Fc iliondoka na ushindi wa bao 1-0
Kuelekea mchezo huo Simba inaendelea na mazoezi makali ambapo kocha mkuu wa mabingwa hao wa nchi, Sven Vandenbroeck amesema wamesahihisha makosa yliyojitokeza kwenye mchezo uliopita
"Tulifanya makosa machache kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao tulipata alama moja, tumefanyia kazi baadhi ya mapungufu nadhani tutakuwa bora zaidi kwenye mchezo unaokuja," alisema Sven katika viunga vya mazoezi ya Simba, Bunju
Jumamosi huenda baadhi ya nyota waliokosa mchezo uliopita wakiongozwa na Mzambia Clatous Chama, watapata nafasi ya kuanza
Chama hakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kwenye mchezo dhidi ya Ruvu baada ya kuchelewa kujiunga na timu
Simba inahitaji alama 13 kuweza kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo. Wakiwa wamebaki na mechi tisa, wanahitaji kushinda mechi nne na sare moja tu