Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba Senzo Mazingisa amekanusha kuwa klabu hiyo imemtuma Wakala kumshawishi mchezaji wa Yanga Barnard Morrison aweze kusaini Simba
Sauti inayodhaniwa kuwa ya Morrison imevuja kwenye mitandao ya kijamii akidai kufuatwa na Wakala aliyetumwa na Simba akampatia dola elfu tano ili kumshawishi nyota huyo aweze kusaini Simba
Morrison alidai kuwa Wakala huyo alimwambia kuwa fedha hizo zimetoka kwa Rais wa Simba
"Klabu ya Simba haina wakala ambaye wanafanya naye kazi kwenye Usajili, lakini pia hatuna cheo cha Rais bali tuna Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Mtendaji Mkuu wa klabu ambaye ni mimi," alijibu kwa kifupi Senzo
Morrison amekuwa akihusishwa na Simba ingawa taarifa hizo bado hazina uthibitisho
Morrison alisaini mkataba wa miezi sita na Yanga ambao unamalizika mwezi Julai na inadaiwa pamoja na kupewa ofa ya mkataba mpya, bado hajasaini
Hivi karibuni aligoma kusafiri na timu hiyo mkoani Shinyanga huku akiwazimia simu viongozi wa Yanga