Luis Miquissone amejizolea sifa kemkem katika kikosi cha Simba tangu alipotua mwezi Januari usajili wa dirisha dogo
Amekuwa na mwanzo mzuri na mabingwa hao wa nchi mpaka sasa akiwa amefunga mabao matatu kwenye ligi
Hakuna shaka kesho Jumapili, atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoikabili Ruvu Shooting katika mchezo wa kwanza kwa Simba baada ya ligi kurejea
Miquissone ametamba kuwa wako tayari kuwapa furaha mashabiki wa Simba hapo kesho kwani 'walimiss' kucheza mpira
Mwamba huyo kutoka nchini Msumbiji amesema baada ya kufanya mazoezi kwa wiki mbili, sasa wako tayari
"Sisi wachezaji tuko tayari kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa kurejea kwa ligi. Tunafahamu mechi itakuwa ngumu na ligi kwa ujumla lakini kama mabingwa tumejiandaa kutetea taji letu," Miquissone aliiambia tovuti ya Simba
"Tumejipanga kuwapa burudani mashabiki watakaojitokeza uwanjani na hii ndiyo kazi yetu tuliwakumbuka na 'tulimiss' kucheza mpira pia"
Simba itaingia kwenye mchezo wa Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa uwanja wa Uhuru
Katika mchezo huo, shoo ilikuwa na Miraji Athumani 'Sheva' ambaye alifunga mabao mawili na jingine likiwekwa kambani na Tairone Da Silva
Ni katika mchezo huo Miraji alipata majeraha yaliyomuweka nje kwa zaidi ya miezi minne na sasa yuko tayari kurejea uwanjani na pengine anaweza kuanza nao Ruvu Shooting kama itampendeza kocha Sven Vandenbroeck