Kasi waliyoonyesha wachezaji wa Simba katika mechi zao za kirafiki dhidi ya Transit Camp na KMC mapema wiki hii na mazoezi yanayoendelea, imewafanya mabosi wa klabu hiyo kujikuta wakikenua na sasa kutamba kubakiwa na jambo moja tu kuufunga msimu kibabe.
Kabla ya timu hiyo kuanza mazoezi, kulikuwa na hofu miongoni mwa wapenzi wa Simba kuwa huenda wachezaji wao wakirejea kizembe baada ya kuwa mapumzikoni kwa muda mrefu.
Tangu Ligi Kuu Tanzania Bara na michezo mingine kusimamishwa Machi 17, mwaka huu kutokana na hofu ya kuenea kwa maambukizi ya virus vya corona, wachezaji walikuwa wamepumzika makwao.
Hata hivyo, wapo ambao walikuwa wakijifua kivyao kwa kufuata masharti ya kuepuka mikusanyiko kama inavyoshauriwa na wataalmu wa afea kulingana na program walizopewa na makocha wao.
Lakini wapo ambao walionekana kutojifua kivile, hali iliyozua hofu kwa makocha wao na hata mashabiki.
Kwa upande wa Simba, idadi kubwa ya wachezaji wameonekana kuwa fiti na hilo limethibitishwa kupitia mechi zao hizo za kirafiki na hata mazoezi yao yanayoendelea kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju, Dar es Salaam.
Pamoja na kucheza mechi mbili kwa siku moja, asubuhi na jioni, lakini bado wachezaji wa Simba waliweza kupambana na kupata ushindi mnono, wakianza na mabao 4-2 dhidi ya Transit Camp, kabla ya kuipiga KMC mabao 3-1.
Hata katika mazoezi, wachezaji wanaonekana kuwa fiti, wakijituma vilivyo kiasi cha kuwafurahisha makocha wao, Sven Vandenbroeck na msaidizi wake, Seleman Matola.
Na sasa mabosi wa Simba wanaamini hawana hofu tena juu ya azma yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo, wanapoelekea kuivaa Ruvu Shooting wikiendi hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kabla ya hapo, wapo waliokuwa wakihofu huenda Ruvu Shooting ikawasumbua kutokana na ukweli kuwa wapinzani wao wanaonekana kuwa fiti, wakiwa wameanza mapema kujifua.
Lakini kwa viwango vinavyoendelea kuonyeshwa na wachezaji wa Simba, mabosi wa klabu hiyo wanaamini lazima wataichapa mabao mengi tu Ruvu Shooting kabla ya kuendeleza vipigo katika mechi zao zijazo za ligi.
"Ukweli ni kwamba tulikuwa na hofu sana na viwango vya wachezaji wetu kutokana na kuwa mapumziko kwa muda mrefu," mmoja wa mabosi wa Simba aliliambia gazeti la Bingwa
"Halafu kitendo cha Ruvu Shooting kutamba kuwa wanataka kuanza kucheza na sisi mchezo wetu wa kiporo, nacho kilituongezea hofu. Tulihisi huenda hawa jamaa wakatutia nuksi iwapo watatufunga na kujikuta tukichanganyikiwa na kuendelea kufanya vibaya.
"Lakini baada ya mechi mbili za kirafiki tulizocheza na hata mazoezi yanayoendelea, tumebaini vijana wetu wapo fiti na walikuwa wakifuata program za mazoezi walizokuwa wkaipewa na walimu wao.
"Kwa sasa hatuna presha, tumebakiwa na jambo moja tu muhimu ili kuufunga msimu kwa kishindo, kutwaa ubingwa wa FA (Kombe la Shirikisho la Azam Sports-ASFC) kwani uhakika wa kombe la Ligi Kuu tunayo.”
Alisema kuwa lengo lao ni kuhakikisha Yanga wanatoka kapa msimu huu na kukosa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao hali itakayoongeza furaha kwao na wapenzi wa Simba kwa ujumla