Siku moja baada ya TFF kuizuia klabu ya Simba kuutumia uwanja wake wa Mo Simba Arena kwa ajili ya michezo ya kirafiki, uongozi wa mabingwa hao wa nchi umewataka mashabiki wanaojitokeza kuwaunga mkono kuhakikisha wanafuata taratibu zote zilizotolewa na serikali kupitia Wizara ya Afya kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa corona
Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema ni vyema mashabiki wakaendelea kuchukua tahadhari wakati wote kama ilivyoelekeza Serikali pale wanapojitokeza viwanjani kuiunga mkono timu hiyo
"Kuanzia Jumapili hii katika mchezo unaofuata wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting na mingine yote iliyosalia mashabiki wote watakaojitokeza viwanjani lazima wanawe mikono"
"Niwatake mashabiki wetu wahakikishe wanafuata taratibu zote zilizotolewa na Wizara ya Afya jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa corona, wavae barakoa na wakiingia viwanjani wakae umbali wa mita moja kutoka mtu na mtu, ni suala dogo ambalo sidhani kama kuna mtu atashindwa.
"Rais wetu John Magufuli anatupenda ndiyo maana ametufungulia kuendelea na Michezo kwa hiyo kama hatutafuata taratibu haitapendeza. Wanasimba ni wasikivu na wastaarabu nina imani watafuata taratibu zote," alisema Manara
Juzi idadi kubwa ya mashabiki walijitokeza uwanja wa Mo Simba Arena kushuhudia michezo miwili ya kirafiki ambayo Simba ilicheza dhidi ya Transit Camp na KMC, michezo ambayo waliishuhudia mbashara bila kiingilio
Baadhi ya mashabiki hawakuchukua tahadhari ya corona kama Serikali ilivyoelekeza hivyo kupelekea TFF kusitisha uwanja huo kutumika kwa michezo ya kirafiki